Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Nyumba 200 zasombwa na mafuriko Pemba

$
0
0

Nyumba 666 zimeathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha kisiwani Pemba, huku nyengine 200 zikisombwa kabisa na kuziacha familia zaidi ya 3,000 kukosa makaazi.

Hayo yalidhihirikia jana baada ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF (Zanzibar), Nassor Ahmed Mazrui, kufanya ziara maalum ya kuwafariji waathirika hao  jana.

Wanakijiji wa Muambe katika mkoa wa Kusini walimuambia Mazrui kuwa licha ya ukweli kwamba mvua za mara hii zimekuwa kubwa kuliko kawaida, lakini pia “uzembe wa serikali kwa kuchimba kusi kwa ajili ya kutengenezea barabara na kisha kuyaacha mashimo makubwa” ambayo sasa yamejaa maji.

“Japo mvua ni sababu, lakini serikali nayo imechangia, kwani tuliwaeleza kuwa wasituchimbie fusi karibu na majumba, lakini hawakukubali. Leo hii maji yamejaa hayana njia yamekuja majumbani mwetuu,” alieleza Seif Khamis Mohammed, ambaye ni mkaazi ya kijiji hicho.

Click to view slideshow.

Mohammed alifahamisha kuwa katika eneo hilo pekee, nyumba 62 zimeanguka kutokana na mvua hizo na wakaazi wake kupewa makaazi katika majengo ya afisi mbalimbai, zikiwemo za CUF.

Aidha alieleza khofu yao kubwa ni kukumbwa na maradhi ya mripuko hasa kipindupindu kutokana na kuzagaa kwa uchafu kwenye maeneo hayo.

Mkaazi mwengine aliyejitambulisha kwa jina la Shauri Makame Khamis alieleza kuwa katika mashimo hayo walijaribu kupanda migomba lakini haikuwa na msaada kwa tukio hilo.

“Siye tulijaribu kutaka kulizuia lakini juhudi zetu ni za kimasikini, kwa hiyo hatukufanikiwa,” alieleza Khamis.

Baada ya kupata maelezo kutoka kwa wanavijiji mbalimbali, Naibu Katibu Mkuu huzo wa CUF aliwaomba wananchi kuwaangalia wenzao waliopatwa majanga hayo ili wajione kuwa msiba huo ni wao wote, akiwasisitiza wale wenye uwezo kutoa msaada wa hali na mali hasa katika kipindi hiki, kwani familia kadhaa hazina hata chakula.

“Tunayaomba mashirika ya kutoa misaada kuwaangalia kwa haraka wananchi hawa, kwani hali zao ni mbaya sana na wako katika hali ya kimasikini sana,” alieleza Mazrui.

Sambamba na hilo, Mazrui aliwaomba pia wananchi hao kuwa na ustahamilivu na wasije wakajenga katika maeneo ambayo makaazi yao yalibomoka kwa ambacho mvua inaendelea kunyesha.

Nyumba zaangukiwa na maporomoko ya mlima

Mvua za masika zinazoendelea kunyesha hadi sasa zimeiporomoa hata milima kisiwani Pemba. Nyumba ya Bi Mariam Khamis wa kijiji cha Jondeni iliporomokewa na mlima wakati wenyewe wakiwa ndani wamelala.

‘Tulikuwaa watu watano. Sote tulifukiwa, lakini majirani walisikia mshindo ndio wakafanya jithada za kutuokoa na Alhamdulillah sote wazima isipokuwa mwezetu mmoja hajatoka hospitali, lakini naye anendelea vizuri,” alisema Bi Mariam.

Rashid Khalid ambaye ni mkazi wa Micheweni alieleza kuwa katika wilaya yao hiyo nyumba 59 zimebomoka moja kwa moja kutokana na mvua.

Naye pia alielezea Mazrui masikitiko yake kuwa licha ya hali mbaya ambayo wananchi imewapata, hakuna hata kiongozi mmoja wa serikali aliyefika kuwafariji.

“Lakini juhudi zetu wananchi zimepelekea wenzetu kuwasaidia kwa kuwapatia huduma tofauti ambazo zimo kwenye uwezo wetu,” alieleza Rashid.

Kwa upande wa wilaya za Wete na Chake Chake, nyumba zilizoanguka ni 79, zikiwaacha wenyewe wakihangaika kutafuta wasamaria wema wa kuwahifadhi.

Wataalamu kisiwani Pemba wanasema kuwa mvua inayonyesha mwaka huu haijawahi kutokea ndani ya takribani miaka 30 iliyopita.

TANBIHI: Habari na picha na Talib Ussi


Filed under: HABARI Tagged: mafuriko, mkoani, pemba

Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles