Licha ya mgombea urais wa mrengo wa kati nchini Ufaransa, Emmanuel Macron, kujishindia asilimia 66.1 ya kura kwenye uchaguzi wa duru ya pili hapo jana, dhidi ya hasimu wake wa mrengo mkali wa kulia, Marine Le Pen, aliyepata asilimia 33.9, na ushindi huo kusifiwa kote ulimwenguni, ukweli ni kwamba kuna hatari kubwa kwenye siasa za uchaguzi nchini Ufaransa na ishara mbaya kwa Ulaya nzima.
Wapigakura 4,045,395 waliamua ama kuziharibu kura zao ama kutumbukiza karatasi tupu, yaani kupiga kura za maruhani, huku wengine 11,416,465 wakiamua kutokupiga kura kabisa. Idadi hii inatajwa kuwa haikuwa imetabiriwa na mapema na inatuma ujumbe mzito.
Ingawa kura alizopata Macron (20,257,167) ni mara mbili zaidi ya zile alizopata Le Pen (10,584,646), lakini idadi ya waliomchaguwa Le Pen anayefuata siasa kali za mrengo wa kulia ni kubwa mara mbili kuliko ile iliyomchaguwa baba yake kwenye uchaguzi wa 2002, ambaye naye alifikia duru ya pili kama bintiye. Hii inamaanisha kuwa kuna ongezeko kubwa la waungaji mkono wa siasa kali nchini Ufaransa, kama ilivyo kwenye mataifa mengine ya Ulaya ya Magharibi.
Filed under: HABARI Tagged: Emmanuel Macron, Marine Le Pen, uchaguzi, Ufaransa, Ulaya
