Ni mwaka wa pili sasa kwa Wakfu wa Mo Ibrahim kushindwa kupata mtu wa kumtunuku Tunzo ya Uongozi Bora Afrika. Katika hali ya kushangaza, kamati maalum kwa ajili ya kuteuwa kiongozi wa kumpa tunzo hiyo haijapata kiongozi hata mmoja anayefaa kwenye mataifa 53 ya bara letu hili.
Hii ni baada ya kamati hiyo iliyoongozwa na mwanadiplomasia mbobezi kutoka Zanzibar, Dk. Salim Ahmed Salim, kuja mbele ya hadhira na kutangaza kukosekana kwa mshindi wa kumtunuku tuzo hiyo. Katibu mkuu huyo wa zamani wa Umoja wa Afrika amenukuliwa akisema kuwa baada ya upembuzi wa kina, kamati yake imekosa mshindi.
Katika moja ya vigezo vya kupokea tunzo hiyo, ni kwa kiongozi kuwa amechaguliwa kidemokrasia na kuhudumu kwenye mihula yake ya uongozi kwa kufuata katiba ya nchi yake, akiwatumikia vizuri watu wake na kusaidia katika kupeleka mbele gurudumu la maendeleo katika nchi yake anayoiyongoza.
Lengo la makala yangu sio tu kujadili kwa nini kamati inayoongozwa na Dk. Salim imekosa kiongozi wa kumtunuku tuzo, lakini kuangalia dhana nzima ya uongozi, ustawi wa demokrasia na maendeleo katika bara la Afrika, na jinsi hatma ya bara hili inavyoelekea kusikoeleweka.

Kwa maoni yangu tunzo ya Mo Ibrahim imekosa mtu kwa kuwa hatuna tena viongozi wa Kiafirka wanaojali maslahi ya watu wao. Hilo linathibitishwa na mienendo ya viongozi wengi tulionao sasa. Badala yake, viongozi tulionao ni wala rushwa, mafisadi, wakandamizaji wa haki za binadamu, wasiojua utawala bora, wang’ang’aniaji madaraka kwa mabavu na nguvu, huku wengine wakituhumiwa kuuwa na watumbukizaji nchi zao katika umasikini. Hivi nani mwenye akili timamu atawapa tunzo viongozi wa aina hii? Labda shetani!
Hebu angalia, kwa mfano, hatua ya miezi michache iliyopita pale viongozi wa nchi za Afrika walipokutana Addis Ababa, Ethiopia, kupitisha azimio la kujitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa kile wanachodai kuwa mahakama hiyo inaegemea na kuwalenga zaidi viongozi wao.
Kama kweli viongozi wa Kiafrika wanalengwa na mahakama hii, kwa nini baadhi ya nchi hatuzisikii zikitajwa kwa uhalifu wa aina yoyote? Ikiwa viongozi wa Kiafrika wanajiamini kuwa hawana rikodi za uhalifu, kwanini wawe na hofu mpaka kufikia uamuzi wa kujitoa ICC?
Asiyevunja sheria huwa hana hofu yoyote na sheria au mahakama. Aghlabu wanaoziogopa sheria wanakuwa ndio wavunjaji wakubwa wa sheria zenyewe. Sababu wanazozitoa viongozi wa Afrika kufikia uamuzi huo, zina walakini nyingi na zinatia shaka sana ikiwa ndizo kweli zinazowafanya watake kujiondoa ICC au kuna ambalo wanalificha.
Baada ya zaidi ya nusu karne ya kuwa huru na kuwaondosha wakoloni kwenye bara hili, mtu anaweza kujiuliza ikiwa viongozi wetu wa Kiafirka wana ujasiri gani unaoweza kuwatofautisha na wale walioitwa wakoloni? Unapomsikiliza kiongozi kama Rais Yoweri Museveni wa Uganda akisema waziwazi kuwa yeye sio mtumishi wa mtu, bali anapigania maisha yake binafsi, ndipo unajuwa Afrika imepatikana.
Museveni mwenye kauli kama hizi ni mmoja wa wanaoidharau mno mahakama ya ICC hata kama inamsaidia sasa kupambana na uovu wa kundi la waasi la Lords Resistence Army (LRA), ambalo viongozi wake wakuu wanasakwa na mahakama hiyo ya The Hague. Si ajabu kuwa akiwa wa kwanza kujitoa katika mahakama ya ICC, kwa sababu kauli zake tu zinaashiria kuwa hana dhamira njema kwa watu wake anaowaongoza.
Hii inamaanisha kuwa kutumikia tumbo lake na kutojali watu wake ndio analoliwaza kiongozi tu, na wala sio ajabu kuwa wapo viongozi wengine kama huyu wa Kiafrika. Ni fedheha kiongozi mkubwa kama huyo aliyedumu madarakani kwa muda wa miaka 25 aje na kauli hiyo.
Hii inatoa maana kuwa tuzo mfano wa Mo Ibrahim itaendelea kukosa mshindi, ikiwa viongozi wenyewe ndio kama hawa, pia nchi ambazo zitataka kutoka ICC huenda zikaongezeka kwani wengi hufikiria kubaki madarakani kwa mabavu na mbinu, hivyo mioyo ya kuiogopa ICC ni lazima watakuwa nayo.
Ni jambo la kawaida kwa viongozi wa Kiafrika kujilimbikizia mali, kuhusika katika ulaji rushwa wa kutisha na hata kuhujumu vyama vya upinzani. Mfano ripoti ya Human Rights Watch imezitaja nchi 10 za Kiafrika ambazo serikali zake zinatajwa kuhusika moja kwa moja katika kuhujumu upinzani na harakati za mabadiliko.
Ni wazi kusema kuwa kwa jinsi ya tawala nyingi zilivyo Afrika sasa, ni kazi kubwa kutokea kiongozi atakayepewa tunzo. Unawezaje kumpa tunzo mtu kama Yahya Jammeh na wengine wanaofanya kama aliyofanya yeye?
Asiyekuwa muuwaji basi ni fisadi, kama si fisadi ni chanzo cha matatizo ya kila aina katika nchi yake, nirudie lile nililolisema awali kuwa tawala kama hizi labda ni shetani tu ndio atakuja kutoa tunzo lakini sio binaadamu mwenye akili timamu.
Mashirika mfano wa Human Rights Watch na Amnesty International hayakawii kuja na ripoti zao zinazohusu uvunjifu wa haki za binaadamu Afrika. Kila mwaka ni lazima watoe ripoti za kusikitisha kuhusu haki za binaadamu na utawala bora katika bara la Afrika.
Wala sitaki kuamini kuwa wanatoa ripoti hizo kwa uonevu, sisi ndio Waafrika wenyewe na yaliyomo Afrika tunayajua na kuyaona, watoto wanakufa kwa njaa, watu wanauwawa kinyama, zipo serikali nyingi za Kiafrika ambazo zinatuhumiwa kufadhili makundi ya kuwahujumu raia wao wenyewe, mfano wa lile la Janjaweed lililopo Sudan na mfano kama huo ukiigizwa hapa petu.
Inaumiza unaposoma ripoti za shirika la Transparency International, lenye makao makuu yake Berlin nchini Ujerumani, ambalo huangazia tatizo la ufisadi, mara zote katika ripoti zake mataifa ya Afrika huwa mstari wa mbele katika ufisadi.
Kenyatta anatuhumiwa mauaji, Mugabe anatumia vikosi vyake kuzima upinzani, Jacob Zuma analiliwa na upinzani kwa kutumia fedha za umma kujenga kasri lake, Mohammad Buhari na vikosi vyake ni mara nyingi amewahi kutuhumiwa kukiuka haki za binaadamu katika mapambano yake dhidi ya Boko Haram, mifano ni mingi kuonesha kuwa hakuna uwezekano wa tunzo ya Mo Ibrahim kwa vile tawala zao haziakisi demokrasia na utawala bora.
Wanachokifanya sasa ni kutaka kujitoa ICC ili kama ni ubabe, wizi, uuwaji, ufisadi waufanye kwa wasaa zaidi, kisha kusiwe na mtu wa kuwauliza hata kitu, maana nyingi ya mahakama zetu za ndani hazina meno ya kukemea matendo maovu yanayofanywa na watawala.
Ni jukumu la Waafrika wenyewe kuijenga heshima ya bara hili ili liweze kurudi katika nafasi yake. Kama hilo litashindikina, tusubirie tunzo kutoka kwa mawakala wa mashetani au shetani mwenyewe. Waliojaaliwa akili na wanaoona hali ya mambo inavyokwenda, kila mwaka watakuja mbele ya waandishi wa habari na kutamka lugha ile ile “tumekosa mshindi wa tunzo”.
Filed under: Masuala ya Kisiasa Tagged: Afrika, Mo Ibrahim, Salim Ahmed salim
