Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Sahara Magharibi kama Zanzibar

$
0
0

edfNaandika makala hii nikiwa kwenye ziara ya kikazi nchini Morocco katika mji wa Marrakesh, ambao sehemu yake ya kale ina mengi yanayofanana na ya Mji Mkongwe wa Zanzibar, husemi ila wachoraji wa ramani za miji hii miwili walikuwa wamoja – majumba ya mawe yenye vichochoro na pindo nyembamba, juu yakipambwa kwa viroshani na chini maduka ya viungo, nguo na vyakula.

Lakini makala hii si kuhusu mfanano baina ya miji ya Marrakesh na Zanzibar tu, bali mfanano baina ya siasa za Morocco kama taifa kuelekea Sahara Magharibi na za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuelekea Zanzibar.

Sahara Magharibi yenyewe inajitambua kama dola na taifa huru – au kwa usahihi zaidi, linalotakiwa kuwa huru. Inatambuliwa hivyo pia na baadhi ya mataifa na taasisi za kimataifa, lakini Morocco inaichukulia kama sehemu yake.

Kwa upande wake, Zanzibar inajitambuwa kwa katiba yake kama nchi ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na hivyo ndivyo inavyotambuliwa kisheria ndani na nje ya mipaka yake, lakini siasa za Jamhuri yenyewe kuelekea Zanzibar zinaitambua kama sehemu moja tu ya nchi inayoitwa Tanzania, na wala sio mshirika maalum na wa kipekee wa Muungano. Na hili lina maana kubwa kwenye utekelezaji wa kila siku wa maisha ya dola.

Sasa, Zanzibar na Sahrawi zinatafautiana humo, wapi hasa zinakutana kiasi cha kunipa hoja ya kuandika makala hii? Papo na nitafafanuwa.

Sahrawi, au Sahara ya Magharibi, ilivamiwa na majirani zake wawili kupitia kile kinachoitwa Mkataba wa Madrid wa tarehe 14 Novemba 1975, ambapo mkoloni Uhispania alikubaliana na majirani Morocco na Mauritania kuwa wajiingize Sahrawi punde yeye anapoondoka.

Ingawa mkataba huo haukutambuliwa na Umoja wa Mataifa na hivyo Uhispania ikaendelea kutambulika kama “mlezi halali” wa watu wa Sahrawi, lakini ndio njia iliyotumiwa na Morocco kuendelea kuikalia ardhi ya Sahara ya Magharibi hadi hivi leo.

Wasahrawi waliupinga uvamizi huo dhidi ya nchi yao. Chini ya cha chama chao cha ukombozi, Polisario, walijitangazia uhuru tarehe 27 Februari 1976, wakaiita nchi yao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kiarabu ya Sahrawi.

Umoja wa Afrika unaitambua jamhuri hii na ina kiti chake kwenye makao makuu ya Umoja huo, Addis Ababa, lakini ukweli ni kuwa serikali yake iliyo uhamishoni inatawala robo moja tu ya eneo ambalo inalichukulia kuwa ardhi ya Sahrawi yenyewe na sehemu iliyobakia ikiendelea kukaliwa na Morocco.

Umoja wa Mataifa hauitambuwi rasmi serikali hiyo, lakini kufikia mwaka jana 2016, ilikuwa imeshatambuliwa na mataifa 85, nayo ikiwa na balozi zake kwenye mataifa 18 duniani.

Kwa upande wake Zanzibar iliyokuwa chini ya Himaya ya Uingereza tangu mwaka 1890, ilipata uhuru wake tarehe 9 Disemba 1963. Lakini mwezi mmoja tu baada ya Muingereza kuondoa mkono wake, kulitokea kile ambacho wengine wanakiita “mapinduzi” ya tarehe 12 Januari 1964 na siku 100 baadaye ukaundwa Muungano na jirani yake, Tanganyika. Kuna uhusiano mkubwa baina ya matukio hayo mawili na kile ambacho Morocco ilikuja kukifanya dhidi ya Sahrawi muongo mmoja baadaye.

Morocco ilitumia kisingizio cha Mkataba wa Madrid kati yake na mkoloni, Uhispania, kuingia na kuikalia ardhi ya Sahrawi. Ushahidi uliosajiliwa kwenye rikodi na maandishi mbalimbali unaonesha mkono wa siri wa serikali ya Tanganyika kwenye “mapinduzi” yaliyotokea Zanzibar kwa kisingizio cha maombi ya baadhi ya viongozi wa Chama cha Afro Shirazi (ASP), akiwemo Marehemu Abdallah Kassim Hanga.

Ikimtumia Waziri wa Mambo ya Ndani, Oscar Kambona, Tanganyika iliyaratibu “mapinduzi” hayo na baada ya kuyafanikisha ikaingia kwenye hatua ya pili na inayoonekana kuwa lengo lenyewe, nalo ni kuikalia Zanzibar kwa jina la Mkataba wa Muungano, hali ambayo imedumua kwa zaidi ya nusu karne sasa.

Tangu Morocco iitwaye Sahrawi mara baada ya mkoloni wa Kizungu (Uhispania) kutangaza kuondoka, inaiita sehemu hiyo Jimbo la Kusini la Morocco. Kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yam waka 1977, Zanzibar nayo inatambuliwa kama Tanzania-Zanzibar.

Kuna wengi sana tunaokhofia kuwa lengo la muda mrefu la CCM, chama chenye kiini chake cha nguvu upande wa Tanganyika, ni kuwa na nchi moja, serikali moja, chama kimoja.

Je, kile kinachoitwa hapa “ukaliaji” wa Tanganyika kwa Zanzibar ni sawa na ukaliaji wa Morocco kwa Sahrawi? Ipo tafauti. Kitabu cha Kwaheri Ukoloni Kwaheri Uhuru cha Dk. Harith Ghassany na kile cha Pan-Africanism or Pragmatism. Lessons of the Tanganyika-Zanzibar Union kilichoandikwa na Prof. Issa Shivji, vyote viwili, vinaelezea kwa undani namna dhana za Mapinduzi na Muungano zilivyofanikiwa kuificha hatua ya Tanganyika visiwani Zanzibar kwenye guo la “dhamira njema”.

Dhana hizo zimetumiwa kuuendeleza na “kuulainisha” ukaliwaji huu kwa njia tafauti. Kwa mfano, jina la asili la mkaliaji limebadilishwa kutoka Tanganyika na kuwa Tanzania Bara ili kulijengea uwiano na lile la Tanzania Zanzibar analolitumia mkaliaji huyo kumuita mkaliwaji wake.

Kuna hata hekaya za uongo na kweli kuwa jina lenyewe la Tanzania lilitokana na ubunifu wa kuchanganya majina ya nchi hizo mbili, “Tan-” kutokana na Tanganyika na “-zan-” kutokana na Zanzibar.

Vile vile, serikali ya Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, ambayo ndiyo hiyo hiyo serikali ya Tanganyika, daima imekuwa ikijumuisha watu – japo wachache – kutoka upande wa mkaliwaji ingawa kutoka chama kile kile ambacho kinaratibu mchakato mzima wa ukaliaji wenyewe.

Katika ngazi ya kijamii, raia wanaotoka ardhi iliyokaliwa wana haki zote kwenye ardhi ya mkaliaji, ikiwemo elimu, ardhi, afya na huduma zote za kijamii kiasi cha kwamba wengi wanajihisi wana maisha mazuri zaidi wakiwa huko kuliko wakiwa kwenye ardhi yao ya asili.

Katika suala la kiusalama, ndani ya kipindi hiki cha zaidi ya nusu karne, mauaji yanayoweza kuhusishwa moja kwa moja na ukaliwaji wenyewe ni yale ya mwaka Januari 2001 ambapo watu zaidi ya 40 waliuawa na vyombo vya dola katika kile kinachoelezewa na shirika la haki za binaadamu la Human Rights Watch kwenye ripoti yake “Risasi Zilinyesha kama Mvua” kama mauaji ya makusudi dhidi ya waandamanaji wasio na silaha.

Ukiwacha hayo, utaukuta “ukaliwaji” huu umeratibiwa kwenye kiwango cha juu kabisa cha kisiasa na ndio maana hata wale wanaoupinga, wanafanya hivyo kwa tahadhari ya hali ya juu sana, wakitumia diplomasia, maridhiano na mualaka. Ndio maama ukiulinganisha na ukaliaji wa Morocco kwa Sahrawi, utaukuta huu wetu una afadhali kidogo.

Vile vile, kinyume na jaala iliyoikumba Sahrawi, ambayo uvamizi wa mataifa jirani dhidi yake ulilaaniwa haraka na Umoja wa Mataifa, kukaliwa kwa Zanzibar na jirani yake hakujawahi kulaaniwa na Umoja wa Mataifa, bali kinyume chake ni kuwa kulikubalika na kupongezwa kuwa mfano bora wa namna nchi za Kiafrika zenyewe zinavyoweza kuihuisha ndoto ya “Afrika Moja”.

Moja ya sababu ni kwamba kilichofanywa na Tanganyika kilipata baraka za wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambao walikuwa na maslahi yao kwa ukaliaji huo na pia kilipitia mikononi mwa kiongozi ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kiakili, Julius Nyerere, kuliko wenzake wa Mauritania na Morocco wa wakati huo walipokuwa wakiivamia Sahrawi.

Kwa hivyo, sharia za kimataifa zinaonekana kuitambua Zanzibar kama nchi iliyomo ndani ya nchi na sio nchi ambayo imekaliwa na nchi nyengine. Nyaraka za Makubaliano ya Muungano na Hati ya Muungano zinatumiwa kama ushahidi wa kuilindia hoja hiyo.

Panatumika pia hoja kuwa madhali hakuna upande ambao umekwenda mahakamani kupinga “ukaliwaji” huu muda wote wa uhai wake na kushinda kesi hiyo, basi kilichopo ni halali moja kwa moja. Lakini je, ni kweli kuwa hakujawahi kufunguliwa kesi dhidi ya hali hii?

Jibu ni kuwa si kweli. Wazanzibari wamethibitisha mara kadhaa kuyatambua mahusiano kati ya nchi yao na Tanganyika kuwa ni mkaliwaji na mkaliaji. Majaribio mengi yamefanywa ndani na nje ya Zanzibar kuiwasilisha picha halisi kisheria, kisiasa na kidiplomasia.

Bahati mbaya ni kuwa sikio la kuyasikia matakwa ya Wazanzibari kwenye hili halijakuwepo. Lakini mjadala ulikuwepo, upo na utaendelea kuwapo, madhali tu dhati ya mahusiano kati ya pande hizi mbili ina walakini mkubwa zaidi kuliko hiki kinachoonekana kwa macho yetu. Kwamba kinachoonekana kwa macho ni “mapinduzi” na “muungano”, lakini kiuhalisia hasa kilichopo ni “uvamizi” na “ukaliwaji”.

TANBIHI: Makala hii ilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye gazeti la Mwelekeo la tarehe 11 Aprili 2017


Filed under: Kalamu ya Ghassani Tagged: jamhuri ya muungano wa tanzania, Morocco, Sahara Magharibi, sahrawi, Tanganyika, Tanzania, Zanzibar
Vyakula vya Marrakesh
Marrakesh Mji Mkongwe

Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles