Wazazi wangu, Mervyn na Auderey Smithman, walikwenda Tanganyika mwaka 1946 baada ya vita kutokea katika Serikali ya Kikoloni ya Muingereza. Baba yangu alikuwa na cheo cha luteni kanali katika jeshi la kikoloni la Uingereza katika Afrika ya Mashariki (Kings African Rifles). Alitokea Nyasaland (Malawi) na alikuwa na uwezo wa kuzungumza lugha ya Chinyanja, kwa hivyo aliweza kujifunza lugha ya Kiswahili na kuzungumza kwa ufasaha. Mama yangu alikuwa mwalimu wa masomo ya Jiografia na lugha ya Kifaransa.
Nimezaliwa Mwanza, Ziwa Viktoria ambako ndiyo sehemu ya kwanza baba yangu aliyofanya kazi. Familia yetu iliishi sehemu nyingi za Tanganyika, ambako baba alishikilia nafasi mbalimbali za kisiasa: Bukoba, Biharumulo, Same, Dare es Salaam, Mbeya; na mwishowe tulihamia Zanzibar mwaka 1956.
Katika miezi sita ya awali, tuliishi Pemba ambako baba yangu alikuwa mkuu wa wilaya. Kwenye kitabu cha kumbukumbu za maisha yake, baba yangu anakumbuka vizuri jinsi tulivyoishi maisha mazuri Chake Chake. Kama Mwakilishi wa Serikali ya Kiingereza huko, alihudhuria sherehe ya harusi ya Bwana Hassan Bin Ali Mahadhiy. Baada ya hapo tulihamia Mji Mkongwe, ambapo mwanzoni baba yangu alikuwa kamishna msaidizi mwenye dhamana ya sensa ya watu na makaazi ya mwaka 1958.

Tuliishi Mazizini kabla ya kuhamia Kikwajuni na miaka yetu ya mwisho Zanzibar tuliishi Shangani pembeni mwa upwa wa bahari, karibu na Mahakama Kuu ya Zanzibar, eneo ambalo lilikuwa zuri kwa watoto. Mimi na kaka yangu tulikuwa na baiskeli na tulikuwa huru kutembea huku na kule. Tuligundua kuwa Wazanzibari ni watu wenye asili ya mchanganyiko mkubwa, wakarimu, wenye furaha pamoja na uvumilivu.
Nilijifunza kuogelea maeneo yenye mandhari nzuri ya bahari na nilitumia muda mwingi nikifurahia na kujirusharusha katika bahari mbele ya eneo la Mambo Msiige. Tulijifunza kuendesha boti kuanzia bandarini Zanzibar kuelekea Kisiwa cha Changuu na kurudi nchi kavu. Tukikumbuka enzi hizo, tunaona kuwa huo ulikuwa ni muda mzuri kwetu na wa kujivunia. Tatizo kubwa kwetu sisi watoto lilikuwa ni kupelekwa katika skuli za dakhalia.
Kaka yangu, Michael, akawa mchezaji mzuri wa kriketi na alikuwa akicheza katika Klabu ya Wazungu hapo Mnazi Mmoja pembeni ya bahari. Nakumbuka watoto walivyocheza mchezo wa kriketi na baba zao hapo Mnazi Mmoja. Baadaye, Michael alikwenda Afrika ya Kusini kucheza katika timu za Chuo Kikuu cha Afrika ya Kusini na timu ya Natal “A”. Alitembelea Uingereza akiwa na timu ya wavulana wa Afrika ya Kusini wakiwemo Mike Proctor na Barry Richards; timu za vyuo vikuu vya Afrika ya Kusini na timu ya Colin Wesley. Huko Uingereza alicheza katika uwanja wa Lord’s Cricket dhidi ya timu nyengine nakumfunga Peter May, aliyekuwa Nahodha wa Uingereza.
Mama yangu alikuwa akisomesha somo la Jiographia katika skuli ya Agha Khan kuanzia mwaka 1961 hadi 1962. Mama yangu aliamini juu ya umuhimu wa elimu na naelewa kuwa alichaguwa kufundisha skuli zenye kiwango cha juu.
Kama watoto tulipendelea sana kwenda Majestic kuangalia sinema. Tulikuwa tukinunuwa njugu mbichi kutoka kwa wafanyabiashara nje ya Majestic na pia tukinunua tiketi za sehemu ya juu za sinema.
Nafikiri tiketi ilikuwa ni shilingi mbili. Nafasi za chini zilikuwa ni za bei rahisi sana. Nakumbuka tulivyokuwa tukisiamama ulipopigwa wimbo wa taifa wa Uingereza. Mara nyengine tulikwenda kuangalia filamu za Kihindi na wale waliokuwa wakiangalia sinema sehemu ya chini walitukera pale walipokuwa wakiwapigia makofi wacheza sinema wa Kihindi!
Nilizifahamu sana njia zote za Mji Mongwe. Nilipendelea Mtaa wa Wareno (Mtaa wa Gizenga), mtaa mkubwa ulikuwa na maduka yaliyojaa masonara wa dhahabu, fedha, pembe za ndovu na baadhi ya vito vya mawe ya thamani kutoka India na Ceylon. Bei zilipanda sana zilipowasili meli za Uingereza.
Baba yangu alijihusisha sana na siasa na ndiye aliyechangia kupatikana kwa Uhuru wa Zanzibar wa mwaka 1963. Mwaka 1959, aliongoza kamati iliyowapa wanawake wa Zanzibar haki ya kupiga kura. Mwaka 1960, aliandika ripoti iliyohusu Maendeleo ya Serikali za Mitaa Zanzibar.
Baba yangu alitakiwa na Sultan wa Zanzibar kusafiri hadi Kisiwa cha Fungu Mbaraka kusini mwa Unguja kwenda kuweka bendera ya Zanzibar kuashiria kuwa kinamilikiwa na Zanzibar. Baba yangu alitunukiwa nishani ya juu na Sultan Sayyid Khalifa bin Harub.
Awali mpango wa Uingereza ulikuwa ni kulekea katika demokrasia pana, lakini kwa vile kipindi hiki kilikuwa cha Vita Baridi kulikuwa na msukumo mkubwa wa harakati za kupigania uhuru kwenye makoloni. Mabishano ya kisiasa yalikuwa ni makali kwa umma. Vyama vikuu vya ZNP/ZPPP pamoja na ASP vilikuwa katika upinzani mkubwa.
Professa J. Glassman anaziita hizi kuwa “Zama za vita vya maneno, vita vya mawe” na hii ilitokana na ukweli kuwa uungwaji mkono wa vyama hivyo ulikuwa ni wa nusu kwa nusu. Hali haikuweza kutabirika.
Baba yangu alikuwa ni msaidizi wa Kamishna wa Tume ya Katiba chini ya Bwana Hilary Blood, wakati alipokuja Zanzibar kupendekeza muundo wa mwisho wa baraza la kutunga sheria. Kwa bahati mbaya, Bwana Blood alitilia mkazo uwepo wa viti 22 vya kuchaguliwa (ambapo kati ya hivyo 8 viti nane vilikuwa ni vya kuteliwa katika hatua hiyo), jambo ambalo lilipekea kuzuka kwa ghasia baada ya uchaguzi wa mwaka 1961.
Mwaka 1962, Waziri wa Uingereza, Bwana Duncan Sunday, alipoitembelea Zanzibar alitangaza kuwa sasa Uingereza ingeliruhusu mfumo mpana wa kidemokrasia. Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 1963 yalileta mshangao mkubwa, muungano wa ZNP ulipata ushindi chini ya asilimia hamsini 50% ya kura zote halali – wakati kwa ukaribu waliweza kushinda kwa viti vingi vya majimbo. Baba yangu akateuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Waziri Mkuu, Mohamed Shamte.
Sikuwepo Zanzibar wakati wa sherehe za Uhuru wa Disemba 1963 ambapo Mwana Mfalme Phillip alikuwa mgeni rasmi. Wazazi wangu walihusika katika sherehe zote za Uhuru. Mwakilishi wa Uingereza, Bwana George Mooring, aliondoka Zanzbar na ndege pamoja na Gordon Highlandere. Bendera mpya ya Zanzibar ikapepea.
Nilikuwa nyumbani kwetu usiku wa Mapinduzi wa Januari 12, 1964. Baba yangu alitumia muda mrefu akiwa katika mazungumzo ya simu akijaribu kutafuta msaada wa kijeshi kutoka kwa jirani zetu (Kenya na Tanganyika) na hata Uingereza ambao walikuwa na mkataba wa pamoja wa ulinzi. Zanzibar haikuwa na jeshi kwa wakati huo. Kwa masikitiko, maombi yote yalikataliwa. Alijaribu pia kutafuta msaada wa jeshi kutoka Pemba, lakini uwanja wa ndege ulikuwa umeshavamiwa.
Nilikuwa na miaka 16 na usiku huo nilitakiwa kukaa juu ya varanda ya nyumba yetu kuangalia makundi yoyote yatakayokaribia katika bustani yetu. Kisa kizima cha matukio haya nimesimulia katika riwaya yangu iiitwayo “Zanzibar Uhuru”.
Wanawake wengine waliokuwemo katika nyumba yetu walisubiri katika eneo la ufukwe wa bahari katika mashua yetu ndogo. Baba yangu alisema kuwa utulivu umerudia ndani ya Mji Mkongwe.
Ilipoonekana wazi kuwa matumaini yote ya kupata msaada kutoka nje yamepotea, baba yangu alikwenda katika Meli ya Salama akitumai kuwa Baraza la Mawaziri lilikuwa huko likiwa kama chombo cha usuluhisi kujaribu kutafuta suluhu na serikali ya waasi. Cha kusikitisha, Baraza la Mawaziri liliukataa ushauri wa baba yangu na likavamiwa.
Hatimaye, Sultan Jamshid na familia yake walikuwa katika meli baada ya kushawishiwa kwa muda mrefu waondoke. Sultan alikuwa anataka kubakia aendeleze mapambano. Baba yangu alisafiri kwenye Meli ya Salama pamoja na Sultan na watu wengine ambao walikataliwa kuingia nchini Kenya. Hatimaye Uingereza ikaandaa mazingira salama yaliyowawezesha kuingia nchini humo.
Matokeo yake ni mauwaji ya kinyama yaliyoongozwa na John Okello yaliharibu kabisa historia ya visiwa hivi.
Kwa kumalizia kisa chetu, familia yetu ilihamia Afrika ya Kusini. Mama yangu alifariki dunia akiwa bado kijana na baba yangu akaowa mke mwengine. Nilikwenda katika Chuo Kikuu cha Durban nilikosomea ualimu, niliolewa na kupata mtoto wa kike na wa kiume. Nilipofika miaka 40, kulikuwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe Afrika Kusini na mimi na mume wangu wa pili tulihamia nchini Australia.
Tokea hapo, nimeandika riwaya kuhusu Zanzibar kuelezea historia ya miaka 50 iliyopita. Naamini Wazanzibari waliteseka sana baada ya mwaka 1964. Pia niliandika historia inayohusu maisha ya baba yangu.
Kwa huzuni kubwa, baba yangu alifariki katika makazi yake huko Chester, Uingereza, mwaka 2008 akiwa na umri wa miaka 97. Kwenye droo ya kitandani mwake alikuwa na kasha la karafuu. Baba yangu alikuwa Muafrika kwenye moyo wake, alikuwa mkweli na muaminifu. Alikuwa muhimili wa siasa za Zanzibar, aliyejitahidi kufanya vyema hata katika vipindi vigumu.
Natambuwa namna nilivyobarikiwa kwa kukulia Zanzibar. Sio tu kwa kuwa ni sehemu iliyopendeza na ninayohisi kuwa na muunganiko nayo kwenye siku zangu za utotoni, bali Zanzibar imekuwa pia na msukumo mkubwa katika maisha yangu kwa njia nyengine nyingi.
Makala hii imeandikwa na Anne Chappel (Smithyman), chini ya anuani “MY ZANZIBAR RECOLLECTIONS”, ambaye pia ni mwandishi wa riwaya ya Zanzibar Uhuru: Revolution, Two Women and The Challenge of Survival … , anapatikana kwa barua pepe: chappels@bigpond.net.au. Makala hii imetafsiriwa kwa Kiswahili na Mohamed Aliy
Filed under: Masuala ya Kijamii Tagged: Anne Chappel, Auderey Smithman, Jamshid, Mapinduzi, Mervyn Smithman, Uhuru, Zanzibar
