Kuna utaratibu wa skuli kuwa na sentensi yake maalum ya kuwavutia watu katika elimu. Sentensi hii huitwa ‘kaulimbiu’ au kwa lugha ya Kiingereza huiutwa “motto”. Iwe ya serikali au ya mtu binafsi, kaulimbiu kwenye skuli ina maana kubwa kwa falsafa ya walioanzisha skuli hiyo.
Hebu tazama baadhi ya kaulimbiu zinazotumiwa na maskuli mbalimbali hapa Zanzibar hivi sasa: “elimu ni nuru”, “Elimu ni ufunguo wa maisha”, “elimu ni hazina”, “elimu ni shindi”, “limu ni msingi wa maisha”, na nyengine kadhaa wa kadha. Haya ni maneno yanayotoka katika akili za watu wenye hekima kwa ajili ya kuonesha umuhimu wa elimu, hivyo hutumika kuwajenga matumaini wanafunzi na wazazi wao juu ya elimu bora inayopatikana skulini hapo na umuhimu wake ili waweze kufikia malengo yao kimaisha. Malengo yoyote mtu anayojiwekea, basi yanamuhitaji awe na hamasa inayomjenga kuyafikia.
Naamini kila mwanadamu anapenda kusoma au kuendelea kimasomo, lakini kutokana na vikwazo kadhaa katika maisha ya awali ya kimasomo, watu wengi wanakosa motisha ya kuendelea na masomo. Wengine hukabiliwa na ugumu wa maisha, wengine huwa hawana ufahamu mzuri, wengine huwa na maisha mazuri na fahamu nzuri lakini makundi anayoambatana nayo humfanya aamini kuwa elimu haina maana yeyote au wengine huona mifano ya waliofanikiwa kwa elimu zao ni wachache na hivyo wakaamua kutokushughulika sana na masomo, bali kushughulika na njia za mkato za kufanikiwa kimaisha.
Hayo na mengine, naamini, ni sababu zinazopelekea elimu yetu kushuka, kuporomoka na kudidimia na matokeo yake kufeli kwa wingi wanafunzi katika shule zetu za Unguja na Pemba. Lakini ninaamini pia kuna jambo ambalo, kando ya kaulimbiu za skuli, kando ya jitihada za walimu na wazazi kwa watoto wao, ambalo linaweza kusaidia kurejesha thamani ya elimu akilini mwa watoto hawa. Jambo hilo ni taswira njema ya wanafunzi waliofanikiwa waliopita kwenye skuli hizo.
Walimu wa skuli wanafahamu historia za wanafunzi wengi waliowahi kuwasomesha au kupitia skulini mwao. Walimu wanafahamu mwanafunzi fulani alikuwa mzito kiufahamu katika masomo yake, lakini ikafika siku kwa bidii aliyokuwa nayo akafaulu na kufika mbali kielimu na hatimaye kufanikiwa kimaisha kupitia elimu. Walimu pia wanafahamu wanafunzi waliokuwa na mazingira magumu kimaisha, lakini hawakukata tamaa, wakajiburura hivyo hivyo na hadi kufikia hatua ya kufanikiwa kielimu, licha ya kuwa na mazingira magumu kimaisha. Pia walimu wanaelewa kwamba kuna wanafunzi waliokuwa watukutu, lakini hatimaye waliendelea kimasomo na kufanikiwa kielimu na kimaisha.

Kama nilivyoeleza awali, kuna mazingira ambayo yanasababisha watu au wanafunzi kuyaacha malengo yao kielimu kwa kuwa wamekosa hamasa ya kielimu, aidha kwa kutoamini juu ya elimu, kuwa na mazingira magumu kimaisha au hata kwa kutoona mtu aliyefanikiwa kimaisha kupitia elimu na ambaye ametoka katika skuli anayosoma yeye.
Sasa ili kuwasaidia wanafunzi na ndugu zetu katika kuyaweka hai matumaini yao ya kielimu, tunapaswa kuwajengea motisha kwa skuli zetu hizi kuanzisha utaratibu wa kuwatafuta wanafunzi wa zamani ambao sasa wamefika mbali kielimu na kufanikiwa kimaisha na historia zao kuandikwa rasmi kwenye skuli hizo.
Ushauri wangu ni kuwa historia hizo zibakie maskulini ili zitumike kuwajenga hamasa ya kimasomo wanafunzi waliopo sasa kwa kuona kwamba kumbe na wao kupitia elimu wanaweza kuwa kama kama hao wenye historia hizo.
Kwa mfano, katika Skuli ya Chokocho iliyo Mkoani, Pemba, patengwe chumba maalum chenye picha za waliosoma hapo, na ndani yake mutolewe maelezo ya awali ya watu hao hadi hapo walipo sasa. Katika Skuli ya Makunduchi, patengwe pia chumba maalum na picha za watu waliosoma hapo na wakafanikiwa kisha ikaeleza maisha yao ya awali na hadi sasa. Hali hiyo pia iwe kwa Skuli ya Mtambwe na nyengine kadhaa wa kadha hapa Zanzibar, ambazo zimetoa wanafunzi waliokuja kuwa watu wakubwa kwenye jamii yetu.
Nasema hivi kwa kuwa naamini katika kila skuli kuna historia ya wanafunzi waliofanikiwa, hivyo kuzidumisha historia zao kuna umuhimu mkubwa wa kuwavutia wanafunzi wa sasa kuangalia taswira njema ya huko mbeleni. Tukumbuke kuwa historia inaweza kuwa sababu moja ya kumtoa mtu sehemu moja na kumsafirisha hadi sehemu nyengine kwa kuangalia kilichofanyika wakati uliopita na kuangalia kinachofanyika sasa na kujiwekea malengo ya baadaye na akayafikia.
Filed under: Masuala ya Kijamii Tagged: skuli, zanzibar. elimu
