
NILIPATA kusema kuwa Jecha Salim Jecha amejidhalilisha, amejidharau na kujishusha hadhi. Haaminiki tena pamoja na kuwa ni mstaafu kiutumishi. Alistaafu utumishi serikalini kwa mujibu wa sheria, akiwa ametimiza umri wa miaka 60 miaka kadhaa iliyopita, lakini amejiingiza katika kusema asichokiamini.
Haoni aibu wala tatizo kudanganya. Alizuga kwa staili ya kujitia hamnazo siku ile ya 28 Oktoba 2015, alipotoa tangazo la kufuta uchaguzi mkuu wa Zanzibar, akiwa chini ya ulinzi wa dola ilhali alijua hakuwa na mamlaka ya kisheria ya alichokifanya. Wala hakujali kama alijishusha na hajasafika.
Bado anaendelea kuzuga watu hata leo, katika jitihada zake dhaifu za kutetea upuuzi ule ulioelekeza kuilazimisha nchi kuingia kwenye balaa la damu; mwenyewe akidai ndio alikuwa anaiokoa nchi na balaa.

Alifuta uchaguzi wakati alikuwa na uhakika kwamba anadhulumu wananchi haki yao ya kuchagua na hivyo kuamua kwa hiari yao kuongozwa na mtu mwingine asiyekuwa kipenzi chake Dk. Ali Mohamed Shein, anayetoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Jecha alijua hakuna sheria inayohalalisha mtu yeyote au hata hiyo tume anayoiongoza kuufuta uchaguzi ambao tayari umeshafanyika. Alijua hilo, ndio maana alitolea tangazo mafichoni akiwa ametelekeza tume na makamishna wake.
Asiyetulia akili sawasawa kama yeye, anakubaliana naye kuwa uamuzi wa kufuta uchaguzi mkuu uliokuwa huru, wa haki na ambao ulionesha uhalisia wa maamuzi ya wananchi wa Zanzibar – kama vile yeye mwenyewe alivyothibitisha kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari siku ya 26 Oktoba 2015 – uliepusha balaa.
Eti uliepusha balaa kwa sababu Zanzibar haikuingia kwenye machafuko. Kwamba kwa akili yake na hao wenzake, Zanzibar ni tulivu, kwa kuona watu wanaendelea na shughuli zao. Huko ni kuzuga kwa kiwango cha juu.
Andika maneno “uchaguzi mkuu Zanzibar 2015” kwenye zana ya kupekulia taarifa mtandaoni leo, uone kitakachokuja haraka. Nimekuta taarifa ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ya matokeo ya uchaguzi wa rais ambayo yamehakikiwa kutoka baadhi ya maeneo ya Zanzibar.
Majira ya saa 2 usiku, tarehe 27 Oktoba 2015, tume ilikuwa imeshatangaza matokeo ya majimbo 31 kati ya 54 yote yaliyokuwa na idadi ya wapigakura 503,860 walioandikishwa na kuingizwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura la Zanzibar.
Matokeo ya kura za urais yaliyokuwa yametangazwa kufikia muda huo yalionesha:
Jina Chama Kura Asilimia
Khamis Iddi Lila ACT-W 189 0.1
Juma Ali Khatib ADA-TADEA 93 0.0
Hamad Rashid Mohamed ADC 252 0.1
Said Soud Said AFP 223 0.1
Ali Khatib Ali CCK 240 0.1
Ali Mohamed Shein CCM 139,557 57.9
Mohammed Masoud RashidCHAUMMA 257. 0.1
Seif Shariff Hamad CUF 93,699 38.9
Taibu Mussa Juma DM 118 0.0
Abdalla Kombo Khamis DP 86 0.0
Kassim Bakar Ally JAHAZI 227 0.1
Seif Ali Iddi NRA 63 0.0
Issa Mohammed Zonga SAU 127 0.1
Hafidh Hassan Suleiman TLP 107 0.0
Leo, Jecha anapomuita Maalim Seif Shariff Hamad kuwa ni muongo na mtu aliyetangaza matokeo ya uchaguzi yasiyokuwepo popote duniani, anamaana gani kama sio kuzuga? Ila ajue anazuga tu wasiojua na wale wasiofikiri kwa akili zao kama alivyo.
Hata mara moja hawezi kudanganya wale wanaojua, wakiwemo mawakala walioshiriki kazi ya kuhesabu na kuzihakiki kura za urais vituoni. Hakukuwa na kura nyingine zaidi ya hizo zilizosimamiwa na tume anayoongoza na kuidhinishwa na watendaji iliowaajiri kazi.
Jecha hajafaulu kuwazuga watazamaji wa uchaguzi wa ndani ya jamhuri na wale waliotoka asasi za mataifa mengine. Hadanganyi hata watazamaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wala wa Jumuiya ya Ushirikiano ya Kusini mwa Afrika (SADC), ambao wananyamaza tu kwa kuwa hawana uamuzi wa kijasiri.
Kwamba Maalim Seif ni muongo, Jecha anakusema leo ikiwa ni zaidi ya mwaka mmoja tangu alipothibitisha roho yake ilivyo mbaya kwa kiongozi huyo mstaarabu, mtaalamu wa siasa, mwalimu na mtu mwenye mapenzi mema na nchi.
Pemba, kule ambako Jecha bila ya aibu anadai uchaguzi uliharibika, kazi ya kuhesabu na kuhakiki kura za urais ilifanywa kwa uangalifu kama sheria inavyotaka. Waliosimamia ni watendaji wa tume ambao hatimaye walituma matokeo makao makuu ya tume bila kusita.
Tatizo ni pale Jecha ambaye amethibitisha alikuwa akihangaika kuhakikisha anatimiza matakwa ya CCM, alipokuta zaidi ya asilimia 90 ya kura za kisiwani Pemba zilimkataa kipenzi chake.
Hapo ndipo mahangaiko yakaanza. Jitihada za kubadilisha matokeo zilikwama kwani hesabu yote ilikuwa tayari mikononi mwa Maalim Seif kupitia watendaji wake. Hata mbinu za kimafiya za kutaka kutumia mawakala wa CUF ili wapitishe matokeo yaliyopikwa, zilishindwa.
Huyu Jecha amebadilika sana kiutu kwa kweli kiasi cha kustahili kuonewa huruma. Pengine ikielezwa asijifiche na hataguswa, labda atarudi kwenye akili zake ambazo amezifisidi mwenyewe. Ajabu, ni nani ametangaza kumdhuru? Hofu yake na aliowatumikia.
Huku akijua fika kuwa anaishi kwenye makwapa ya dola inayomlinda kwa sababu ya uovu huo wa dhulma alioshiriki kuutenda, amekuja na kioja hicho kupitia mahojiano aliyoruhusiwa kufanya na aliowafurahisha, na kwa sababu wana ‘maguvu’ ya maamuzi.
Jecha alisafiri kwenda Dar es Salaam na kufanya mahojiano na Tido Mhando, mtangazaji maarufu nchini na naibu mkurugenzi wa kituo cha televisheni cha Azam (Azam Tv) kupitia kipindi cha Funguka kinachorushwa kila Jumapili kuanzia saa 3 asubuhi.
Ni katika mahojiano hayo alitoa maelezo ya kuzuga watu. Eti kwamba jazba za kisiasa ndio tatizo la Zanzibar. Kwa hivyo naye alikumbwa na jazba hizo alipotakiwa kueleza huo uharibikaji wa uchaguzi ulikuwa maeneo gani wakati haukuripotiwa kwa muda wote watu wakipiga kura mpaka vituo vilipofungwa?
Kazi ya kuhesabu kura, kuzihakiki na hatimaye kuidhinisha matokeo kutangazwa ilikamilika ndio maana yeye mwenyewe alishuhudiwa akitangaza matokeo ya majimbo yale 31.
Hivi ingekuwa mgombea wa CCM alishinda kura halali, Jecha angethubutu kukimbia kazi ya kusimamia kutangaza matokeo yaliyobakia baada ya hayo 31 kuyatangaza hadharani?
Au je, Jecha angeufuta uchaguzi kama alikuwa na uhakika mgombea kipenzi chake, Dk. Shein, alikuwa na kura kisiwani Pemba za kuendeleza ushindi wa kura za Unguja zilizokwishampatia karibu kura 140,000 (asilimia 57)?
Akili ya kawaida inathibitisha alijiachia kwa raha zake, akajipeleka mikononi mwa watawala waovu na wang’ang’anizi wa madaraka, badala ya kukamilisha kazi aliyoteuliwa kuifanya, na kusoma takwimu ambazo yumkini hata sasa haziamini.
Ukweli huu wa Jecha kuhujumu haki baada ya kifisidi akili zake, utaendelea kumzonga kifuani kadiri anavyojitahidi kuzuga watu. Utamdhoofisha tu kama wanavyoumia walionufaika na hujuma aliyoitenda.
Filed under: Masuala ya Kisiasa Tagged: CCM, cuf, Dk. Ali Mohamed Shein, Jecha Salim Jecha, Maalim Seif Sharif Hamad, Zanzibar
