Quantcast
Channel: Zanzibar Daima – Zanzibar Daima
Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Dhuluma dhidi ya Uamsho itakwisha lini?

$
0
0
Ni zaidi ya mwaka wa tatu sasa tangu dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwakamata viongozi na wafuasi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu visiwani Zanzibar kwa tuhuma za ugaidi. Kwa kila hali, miaka hii mitatu imekuwa ya dhuluma, mateso na unyanyasaji unaofanywa na dola dhidi ya raia hawa kwa jina la sheria. Majanga yanayoikumba nchi yana mizizi mirefu, na mojawapo ni hizi dhuluma wanazotendewa wanyonge na ukimya wetu kama jamii na kama taifa. Hapa tunachapisha barua ya mahabusu hao ujuwe kipi wanakipitia ndani ya kipindi hiki, kisha swali moja linalobakia bila majibu ni je, dhuluma hii itaisha lini?
SONY DSC
SONY DSC

BARUA YA WAZI KUTOKA KWA MAHABUSU WA UTUHUMIWA WA UGAIDI GEREZA LA SEGEREA
 Kumb: DA.13/PI:29,2014/2016
 Mahabusu PI/29/2014
Gereza la Mahabusu
Segerea, Dar es Salaam
28/12/2016
Dar es Salaam
MH. JAJI MKUU,
MAHAKAMA KUU YA TANZANIA,
DAR ES SALAAM- TANZANIA.
YAH: UVUNJWAJI WA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Tafadhali husika na mada iliyotajwa hapo juu.
Mheshimiwa Jaji Mkuu,

Tunaelezea uvunjwaji wa haki za binadamu katika maeneo mawili makubwa, kwa upande wa Mahakama na pili ni kwa upande wa Jeshi la Magereza, hasa kwa Gereza la Mahabusu Segerea, Dar es Salaam.

Tukianza kwa upande wa Mahakama kwa kupitia Mahakama ya Rufaa (TCA), kwa muda wa miaka mitatu sasa kuanzia tarehe 24/12/2014 mpaka leo hii tarehe 28/12/2016, imeshindwa kupanga tarehe ya kusikiliza rufani ya upande ya mashitaka inayopinga maamuzi ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam yaliyotolewa na Mhe. Jaji Dk. Fauzi Twaibu ya kuiambia Mahakama ya Hakimu Mkaazi Kisutu inao uwezo wa kutoa maamuzi kwenye hatua za mchakato wa ufunguaji wa shauri.
Sambamba na hilo, Mahakama ya Kisutu pamoja na kuelezwa na Mhe. Jaji Dk. Fauzi kuwa inao uwezo wa kutoa maamuzi, imeshindwa kutoa maamuzi kwa madai kuwa upande wa mashtaka umekata rufaa.
Vile vile, upande wa mashitaka umekuwa ukitumia mgongo wa kutokamilika kwa upelelezi ili wazidi kutuweka jela kwa lengo la kutukomoa na huku wakiidanganya mahakama kuwa upelelezi utakamilika ”very soon’‘ na huku ikichukua zaidi ya miezi tisa.
Pia Hakimu kuegemea upande mmoja wa wanaoshtakia (Upande wa DPP). Mfano Mhe. Hakimu Mwijage akiwa katika kiti cha uhakimu alitoa maelezo kuwa ”Anaongea kama afisa wa Magereza”, wakati magereza ndio wanaolalamikiwa na yeye akajisahau kuwa ni Hakimu hapaswi kuegemea upande wowote. Hata hivyo, tulimuandikia hakimu mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu kuhusu jambo hili yenye Kumbukumbu Namba DA.10/PI.29.2014/2016.
Mshtakiwa Namba 6
Vile vile, mnamo tarehe 15/12/2016, Mheshimiwa Hakimu Wilbrod Mashauri, tulimlalamikia juu ya vitendo vibaya tunavyofanyiwa na jeshi la Magereza hapa Segerea kwa kupigwa mshtakiwa Namba Sita (6) Mohammed Ishaq Yusuph, PI:29/2014 na kupelekwa chumba cha adhabu kijulikanacho kwa ufupi PC kwa muda miezi mitatu (siku tisiini bila ya mapumziko) huku akikoseshwa matibabu baada ya kujeruhiwa vibaya kwa kipigo na waliompiga ni maaskari aitwaye 2upaki na Bahati.
Kufungiwa kwenye chumba cha adhabu ambacho ni choo kwa muda wa siku tisini bila ya mapumziko ambayo ni kinyume na wanavyoadhibiwa wengine (kila wiki wanatolewa siku moja kama ni mapumziko na vile vile kuyasaidia macho kuona vitu vya mbali kutoka kutizama karibu).
Amezuiliwa kufanya ibada kutokana na kuwekwa ndani ya choo, alichukua mswala ili atandike kwa ajili ya kufanya ibada nao amenyang’anywa na afisa usalama anayeitwa Rashid, pia wamemnyang’anya vitabu alivyokuwa akivisoma.
Mhe. Jaji Mkuu,

Wamewazuia wanafamilia yake kumtembelea na kumletea huduma yoyote kwa muda wa miezi mitatu akiwa ndani ya adhabu.

Hasa ukizingatia ni mgonjwa mwenye matatizo ya kuanguka na kuzimia ambayo ni matokeo ya mateso na vipigo akiwa mikononi mwa Polisi, aliandikiwa akafanyiwe kipimo cha CT-Scan katika Hospitali ya Muhimbili tokea mwaka 2015 mpaka sasa hajapelekwa Hospitali na tarehe 25/12/2016 ameanguka na kuzimia akiwa ndani ya chumba cha adhabu (PC) na hata alipopata fahamu alilejeshwa tena chumba hicho hicho cha adhabu (PC).
Siku tisini za adhabu alizopewa mahabusu Mohammed Ishaq Yussuf amaeanza kuzitumikia kuanzia tarehe 05/12/2016 mpaka tarehe 06/03/2017 ambacho atakuwa akipewa robo ya resheni ya chakula cha mchana na maji ya chumvi lita nne (4) kwa siku.
Maji hayo atakunywa, atatumia kwa choo (kwenda haja) atakogea, lita nne hizi itakuwa ndio kipimo cha matumizi ya maji kwa muda wote wa adhabu wa siku tisini (90) – miezi mitatu.
Mheshimiwa Jaji Mkuu,

Malalamiko haya kuhusu Mshtakiwa Namba Sita (Mohammed Ishaq Yusssuf,) tulipomueleza Mheshimiwa Hakimu Wilbrod Mashauri, alitutaka tuyalete Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam. Lililotushangaza, hakuwauliza Magereza chochote kuhusu tulichokilalamikia, isipokuwa alisema mahakama yake imefungwa mdomo na mikono.

Udhalilishaji gerezani
Mheshimiwa Jaji Mkuu,
Kwa upande wa Magereza, kumekuwa na udhalilishaji uliopindukia mipaka. Utu wa mtu umekuwa haujaliwi, kwani mahabusu wote wanaonekana kuwa ni wahalifu, wakati sheria iko wazi ambayo inaelekeza kuwa mahabusu hatakuwa ni mhalifu hadi pale mahakama itakapomtia hatiani.
Mhe. Jaji Mkuu,
Wakati tukiingia gerezani tarehe 17/07/2014, tulimuomba mkuu wa gereza la Segerea muongozo wa gereza na kurudia kukumbushia kwa mkuu mpya wa gereza hilo. La kusikitisha mpaka tunaandika maandiko haya hatujapatiwa bila ya sababu za msingi isipokuwa tunaambiwa tutii bila shuruti.
Mahabusu kupigwa na kutukanwa matusi ya nguoni haya ni mambo ya kawaida hapa gerezani, huku wenyewe magereza wakiwa wanajisifu kwa kusema hizi rungu walizonazo ZIMEPITISHWA NA BUNGE KWA AJILI YA KUWAPIGA MAHABUSU. Mfano Mahabusu Hassan Khamis (Namba PI:41/2014), siku ya tarehe 21/12/2016 wa Mahakama ya Kisutu amepigwa marungu kadhaa kwa kukutwa na mchuzi. Askari aliyempiga anaitwa 2paki, huku akijisifu kupandishwa vyeo kwa kufanya kazi nzuri.
Mahabusu Kassim Mkadam Khamis alipigwa kwa kukutwa na peni ya high lighter, pia Mahabusu Rajabu, ambaye ni mgonjwa wa ngiri ambaye anakaa Cell Namba Tatu (3) ambayo ni sehemu yanayokaa wagonjwa kesi namba PI:14/2015 tarehe 24/12/2016 pamoja na mahabusu wengine, wakati wa zoezi lao magereza la kusachi mahabusu wote alipigwa sana na kila alipojaribu kusema mimi naumwa alijibiwa hivi ”Wagonjwa wako Muhimbili”.
Mahabusu Salim Ali Salim (Namba PI:41/2014) ambaye amelazwa katika Hospitali ya gereza ijulikanayo Cell Namba Saba (7), alilazimishwa kutoka ndani huku wakijua hawezi. Hata pale afisa wa zamu aliposema muacheni, amri hiyo haikuheshimiwa inavyostahiki.
Je, Mhe. Jaji Mkuu, hivi ndivyo sheria inavyosema pamoja na haki za kibinadamu, mahabusu na wafungwa wa kisiasa?
Mhe. Jaji Mkuu,

Adhabu zinazotolewa hapa gerezani nyingi haziendani na kosa husika na hazitolewi kwa mujibu wa sheria bali ni kwa utashi tu wa watu.

Mhe. Jaji Mkuu,

Mshtakiwa Namba Sita (Mohammed Is’haq Yussuf wa PI:29/2014) adhabu hii aliyopewa kuishi ndani ya chumba cha adhabu kwa muda wa miezi mitatu, siku tisini (90) bila kutolewa na kupewa mlo mdogo usiozidi gramu 80, na huku mahabusu huyu akiwa amesharipoti juu ya suala la afya yake na huku magereza wakiwa na taarifa zake kamili, hapa ni wazi jeshi la Magereza linaendeleza maelekezo walioyaanza Jeshi la Polisi kuhakikisha japo mtu mmoja lazima afariki dunia ndani ya mikono yao.

Kwani adhabu hii hailingani na kosa analodaiwa kulitenda, bali inaonekana wazi kuwa ni chuki ndizo zinashawishi utoaji wa adhabu hiyo ambayo tokea tumefika hapa gerezani Segerea tarehe 17/07/2014 haijawahi kutolewa kwa mahabusu yeyote yule wala mfungwa.
Mhe. Jaji Mkuu,

Mshtakiwa kwa kuliona hilo ameamua kugoma kutokula hicho chakula kidogo na leo hii tarehe 28/12/2016 ni siku ya nne.

Mhe. Jaji Mkuu,

Hata unapodai kumuona mkuu wa greza sisi tunaoitwa ”wapemba” PI.29/2014, nayo ni shida kumuona kwa ajili ya kutoa malalamiko.

Mhe. Jaji Mkuu,

Kumekuwa na kauli mbali mbali za chuki na za ubaguzi dhidi yetu sisi tunaoitwa ”Wapemba”. Kwa mfano siku ya tarehe 05/12/2016, askari anaehusika na kitengo cha upekuzi alimueleza mahabusu Mohammed Is’haq Yussuf  wa PI.29/2014 ambaye ni mshitakiwa Namba Sita kuwa sasa ataruka na Wapemba na hata pale Mohammed alipomueleza kuwa atawaambia wenyewe alijibu ninakutuma ukawaambie ”Wapemba wenzio”.

Siku ya tarehe 15/12/2016, sehemu hiyo hiyo ya upekuzi wakati tukirudi mahakamani, alimuambia Mahabusu Hussen Mohamme Ali kuwa ni mchawi na tarehe 21/12/2016 alimwita Hassan Khamis wa PI.41/2014 kuwa ni mshenzi. Kauli kama hizi tuliziripoti kwa mkuu wa gereza aliepita, ACP Abdallah Kiangi, na zilikoma kwa muda na sasa baada ya utawata huu mpya zimerudi tena kwa kasi kubwa.
Mhe. Jaji mkuu hapa tunajiridhisha kuwa yale maneno tuliyoambiwa na ”Task Force” ya kuwa tumeletwa Tanzania Bara kuja kukomolewa ni ya kweli na huenda hizi chuki na ubaguzi ni sehemu ya maagizo waliopewa Jeshi la Magereza watufanyie.
Mhe. Jaji Mkuu,

Ubaguzi tunayofanyiwa na askari magereza hapa gerezani Segerea hauendani na sera ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. John Pombe Magufuli, aliyoitangaza siku ya Uhuru wa Tanganyika tarehe 09/12/2016 ya kuwa Tanzania ni moja.

Mhe. Jaji Mkuu,

Udhalilishaji huu unaofanywa na Jeshi la Magereza kupitia Gereza la Mahabusu Segerea ni kinyume cha katiba ya nchi, kinyume cha mikataba ya kimataifa ya haki za binadamu, mahabusu na wafungwa wa kisiasa na ni kinyume cha utawala bora wa sheria.

Mhe. Jaji Mkuu

Tunakuomba kwa vile wewe ni ndiyo mkuu wa watoa haki katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na vyombo vingine husika kwa mujibu wa sheria za nchi hapa Tanzania, muunde ”TUME HURU” ili ichunguze usahihi wa tunayoyaeleza ili zichukuliwe taratibu za kisheria kwa kasoro hizi zilizojitokeza ili zisiendelee kuvunjwa haki za binadamu, mahabusu na wafungwa wa kisiasa.

Mhe. Jaji Mkuu,
Kwa sasa tunaishi katika hofu kubwa na hali ya wasiwasi na kuona kuwa usalama wetu uko hatarini kwa namna tunavyotendewa hapa gerezani Segerea. Uongozi wa magereza unapaswa kuwajibishwa kwa madhara yoyote yanayoweza kutupata mbeleni. Magereza kushindwa kutoa muongozo wa maisha ya gerezani ni kubariki kutokujua haki zetu za gerezani na hivyo kila tunachofanyiwa tuone ni sheria kwetu.
Baada ya miaka mitatu kupita wamejaribu kuweka karatasi mbili zinazoonyesha sehemu ya makosa pasi na kuonesha ni nani anapaswa kusimamia mchakato mzima wa kesi kuwa ni Magereza au Hakimu, karatasi hizo mbili hazionyeshi haki wala wajibu wa mahabusu akiwa gerezani.
Tunakutakia kila la kheri na utendaji mwema katika kutekeleza majukumu yako kwa uadilifu.
Kwa niaba ya Washtakiwa wote PI:29/2014 Mahakama ya Kisutu.
Mahabusu Farid Hadi Ahmed 
Gereza la Mahabusu Segerea
Dar es Salaam.
NAKALA
1. Makamu wa Rais Jamhuri ya Muungano Tanzania
2. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Tanzania
3. Waziri wa Katiba na Sheria Tanzania
4. Mufti wa Tanzania (BAKWATA)
5. Kamishna Generali wa Magereza Tanzania
6. Tanganyika Law Society(TLS) Tanzania
7. Zanzibar Law Society (ZLS) Zanzibar

Filed under: Masuala ya Kisiasa Tagged: Tanzania, Uamsho, Zanzibar

Viewing all articles
Browse latest Browse all 854

Trending Articles