Mwaka 2007, nilibahatika kwenda Libya kwa mafunzo ya muda mfupi, wakati kiongozi wa wakati huo, Marehemu Muammar Gaddafi, akiwa kwenye propaganda kubwa ya kuitangaza nchi hiyo kama taifa la mfano lisilofungamana na sera za Mashariki wala Magharibi.
Mwenyewe Gaddafi alikuwa akiamini kile alichokiita “Demokrasia ya Moja kwa Moja”, akipingana na nadharia ya “Demokrasia ya Uwakilishi”, ambapo kiongozi huyo aliyekuwa na sauti kubwa barani Afrika aliamini kwenye kuwashirikisha raia moja kwa moja katika uendesjaji wa nchi yao, akitumia falsafa ya “Mfumo wa Tatu wa Kilimwengu” (Third Universal Theory) inayofafanuliwa vyema kwenye kitabu alichokiandika kwa jina la “Green Book”.
Kitu kimoja lazima nikikiri: kwamba wakati nikiwa Libya, niliikuta nchi hiyo inapiga hatua kubwa za maendeleo. Huduma za jamii zilikuwa zikiwafuata raia kwenye makaazi yao na sio wao kuzifuata zilipo.
Raia wakihimizwa kusoma popote watakapo duniani wakifuata kauli maarufu ya Mtume Muhammad (S.A.W) isemayo “Itafuteni elimu hata kama ni China”, tena wakilipiwa kwa ruzuku za serikali yao. Hakika, Gaddafi alikuwa hata akiwasaidia wanafunzi wa mataifa mengine masikini barani Afrika kusoma kupitia mifuko yake mbalimbali ya misaada. Niliyakuta makaazi ya raia yakiwa yameshataarishwa yakimsubiri kijana atimie miaka 18 akabidhiwe nyumba yake.
Kwa ujumla, Libya ya Gaddafi ilikuwa ni ishara ya maendeleo na ustawi na alama ya kile ambacho kiongozi wa taifa la Kiarabu na Kiafrika anavyoweza kuitoa nchi yake kutoka kwenye masikini kuelekea kwenye uimara wa uchumi na ustawi wa kijamii.
Hata hivyo, pamoja na maendeleo yote hayo, jambo lililokuwa dhahiri katika nyuso za watu niliokutana nao ni khofu. Khofu hii ilitokana na kukosa uhuru wa kutoa maoni yao, kuminywa uwezo wa kufumbua midomo yao na kuwa na mawazo tafauti katika kiwango ambacho hata wakawa hawaaminiani wao kwa wao.
Kwa Libya ya Gaddafi, ilikuwa ni lazima usikilize propaganda za Gaddafi, uzikariri na uzisambaze kwa wengine. Maoni ya mtu binafsi hayakupewa nafasi. Ukitaka kusema tofauti na alichokuwa akikisema Gaddafi, basi ulilazimika kukisema nje ya nchi na kisha baada ya hapo usirudi tena Libya, ikiwa unataka uhai wako. Wengi kati ya walioutamani uhuru wa kutoa maoni, ama walimalizikia kwenye jela za Gaddafi au kukimbia na kuishi uhamishoni.
Kwa upande mwengine, Gaddafi hakuwa kipenzi cha mabwana wa dunia – mataifa ya Magharibi – ambao huenda walimuona kuwa ni kitisho kwa utukufu wao barani Afrika na katika mataifa ya Kiarabu. Alikuwa amejenga nchi kwa mikono na akili yake mwenyewe, hakutaka mikopo wala misaada ya mashirika ya fedha ya kimataifa, badala yake yeye alitaka kuwakopesha wao na, kwa hakika, alikuwa akiwafadhili wanasiasa wakubwa wa Kimagharibi, akiwemo aliyekuwa rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy.
Vile vile, ugomvi wake na Marekani ulikuwa wa siku nyingi na hata alipoamua kusaka suluhu, hawakumsamehe. Walimuonesha kuwa wako tayari kwa maridhiano lakini walikuwa wanasubiri mahala pa kumtia adabu.
Ndipo hili na kunyima watu uhuru, wengine waliliona kuwa litakuwa chachu ya kuwafanya raia wa Libya kumchoka Gaddafi na hivyo wakipata msukumo mdogo wangeweza kuungana dhidi ya kiongozi wao huyo. Na hivyo ndivyo ilivyokuwa pale mwaka 2012 lilipoanza “Wimbi la Mageuzi ya Umma ya Arabuni” (Arab Spring), Walibya wasioridhika na kuminywa uhuru wao, walio ndani na nje, wakaungana kumuangusha Gaddafi. Ghafla moja, wakasahau neema yote waliyoshushiwa na Gaddafi mwenyewe.
Muda wote, Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akipata nafasi, huwa anatuasa tusicheze na amani, na mara nyingi amekuwa akitutolea mfano wa Libya ilivyokuwa wakati wa Gaddafi na ilivyo leo baada ya kuondolewa kwake.
Sijui mfanano anauweka kwenye mantiki yake hii, maana Tanzania aliyoichukuwa yeye kama kiongozi mkuu wa nchi mwaka mmoja uliopita, haina hata robo ya nguvu za kiuchumi na kimaendeleo iliyokuwa nayo Libya ya Gaddafi na bado wananchi hao waliinuka dhidi yake.
Pengine Rais Magufuli hajapata kuzingatia njia aliyotumia Gaddafi kuwatawala Walibya, nami khofu yangu ni kuwa huenda naye sasa anatupitisha njia ile ile ya mfano asioupenda wa nchi ya Libya.
Tanbihi: Mwandishi wa makala hii, Issa Hussein, ni mwalimu kitaaluma na mchambuzi wa masuala ya siasa.
Filed under: Masuala ya Kisiasa Tagged: Gaddafi, Libya, Magufuli
