Kuna mambo ambayo hatupaswi kuacha yapite hivi hivi pasi kuyajadili kutokana na uzito wa kile kilichojiri au mwenye kukiwasilisha kwa hadhira aliyoikusudia. Uzito wa hili la leo upo pande zote – wa mtoaji na wa kile alichokitowa, nayo ni kauli ya Katibu Mkuu wa chama Alliance for Democratic Change, Doyo Hassan Doyo, pale alipoandika kwenye ukurasa wa Facebook kuwa “Upemba ni janga la kitaifa” na hata mwandishi wa makala hii alipomtafuta kumtaka ufafanuzi, akaongeza kuwa sio tu ni janga la kitaifa, bali “Upemba ni janga la Muungano!”
Uwasilishaji ujumbe una njia nyingi kuanzia ile ya maandishi, maneno au ishara na tafauti kati yake ni kubwa na, hivyo pia, athari zake. Kwamba ujumbe unaotolewa kwa maandishi una nafasi kubwa ya kuishi kwa muda mrefu na hivyo kuwa na athari inayoendelea zaidi kuliko ule wa maneno au ishara. Ndio maana manunuzi ya shamba aliyofanya babu yangu mzaa mama mwaka 1948 kwenye kijiji cha Shungi kilichopo wilaya ya Mkoani ya Mkoa wa Kusini Pemba, leo hii upo mikononi mwangu, nami nikiwa mmiliki wa shamba hilo, licha ya kuwa mwaka ambao babu yangu ananunuwa shamba hili, mwanawe (ambaye ni mama yangu mzazi) alikuwa na umri wa miaka mitatu tu. Hata hivyo, mama aliukuta waraka huu na kisha akaurithisha kwangu ambaye sikubahatika kumjuwa babu huyu aliyenizalia mama, lakini nimemilikishwa shamba ambalo mzee wangu huyu alilinua miaka takribani 60 iliyopita!

Ndio maana pia, ingawa wengi miongoni mwetu tunaamini katika dini tulizozichaguwa kuwa waumini wake, lakini hayupo kati yetu aliyepata kumshuhudia Mtume Issa (Yesu) au Nabii Muhammad akifikisha Neno la Mungu, bali ujuzi na uelewa wetu juu ya imani zetu za kidini umetokana na mapokeo yaliyotokana na vitabu vyenye kubeba ujumbe huo wa kiimani.
Mifano yote hii miwili inaonesha namna maandishi yanavyoishi muda mrefu kupita namna nyingine yoyote ya kufikisha ujumbe. Hivyo ni jambo la msingi kwa mtu kuitafakari faida na hasara ya kutumia njia hii pindi akiwa na lengo la kufikisha ujumbe kwa yule aliyemkusudia. Kauli ya Doyo, ambaye chama chake cha ADC kinawakilishwa kwenye serikali ya Zanzibar kupitia mwenyekiti wao, Bwana Hamad Rashid Mohamed, aliye mwakilishi wa kuteuliwa na waziri wa kilimo na mifugo, inasema mengi mabaya kwake na kwa chama chake.
Licha ya makandokando mengi yaliyomo kwenye uwezo wa kisiasa wa chama chenyewe na uhalali wake wa kuwamo kwenye serikali ambayo yenyewe haina uhalali, bado kuna mambo ya kimsingi ya kisiasa ndani yake. Kwanza ni kuwa uwepo wa chama hiki unatambuliwa kisheria. Pili, kutambuliwa huko ndiko kulikokifanya kuwa mshirika kwenye muundo wa serikali iliopo sasa Zanzibar na hivyo kukitowa kwenye nafasi ya vyama vya vichochoroni. Unyeti wa chama hiki hauishii kwenye chama kama taasisi tu, bali hata kwa viongozi wenye dhamana za kiuongozi na majukumu mazito ya kila siku.
Hata hivyo, kwa kauli hii, kinachoonekana ni ukosefu wa hikima miongoni mwa viongozi na wafuasi wa chama hiki, kikichukuwa na kubeba tabia zile zile za washirika wao madarakani, yaani Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho kutoa kauli za kuwadhalilisha, kuwabagua na hata kuwaumiza Wapemba na Upemba wao ni jambo la kawaida. Inawezekana ni yale ya mlipaji mpiga zumari kuwa na nguvu za kuchagua wimbo, kwa maana ya fadhila ya CCM kwa ADC inakipa haki chama tawala kuigeuza ADC kusema yale yale yanayosemwa na maskani za Kisonge na mikutano ya Boraafya Silima, lakini binafsi siioni hikma ya kiuongozi iwapo mtu mwenye dhamana ya ukatibu mkuu wa chama anapata uthubutu wa kuweka hadharani maandishi amabayo yana ishara za wazi za kibaguzi dhidi ya jamii fulani.
Kwa jamii inayoujuwa utamaduni wa kisiasa na kwa kiongozi anayewajibika kwa misingi ya kikatiba na kitaifa, hadi hapa Doyo hastahili tena kuendelea kuwa katibu mkuu wa chama hicho. Kungelikuwa na utamaduni na ustaarabu wa kujiwajibisha, angelipaswa kufanya hivyo. Alipaswa kutoka hadharani kuomba radhi kwa kauli yake hii au vyenginevyo akabiliane na mashtaka kama yalivyowakuta wachochezi wengi ambao walipelekeya maangamizi kwa jamii walizozichukia. Mauwaji mengi Afrika yanayoitwa ya kimbari yalianzia na kauli zisizo busara kama hii.
Kauli kama hii haitegemewi kwa mtu ambaye ameaminiwa kwa dhamana ya ukatibu mkuu wa chama cha siasa ambacho ni mshirika wa serikali iliyopo sasa. Baya zaidi ni kuwa hata mwenyekiti wa chama chake, Bwana Hamad Rashid Mohamed ni Mpemba wa Wawi, wilaya ya Chake Chake. Isitoshe, waasisi wa chama hicho, wakiwemo Bwana Said Miraj Abdullah na Bwana Shoka Hamad, nao pia ni Wapemba fyoko. Lakini chuki zina kawaida ya kupofusha, kama pale akina Borafya Silima wanapopanda kwenye viriri kuwatukana Wapemba, ilhali makamu mwenyekiti wa chama chao, Dk. Ali Mohamed Shein, naye ni Mpemba pia, bali wengine hata wake na watoto wao ni wa Kipemba.
Kauli hii inatowa ishara ya mwanasiasa muflisi au aliye kwenye dhamana ya kiuongozi kwa njia ya sadfa kutokana na hali ya kutokuwepo mwingine wa kukamata nafasi hiyo. Siamini kwamba mheshimiwa huyu ana hadhi au ufahamu wa kutosha kuhusiana na dhima ibebwayo na cheo chake. Huyu bado ni mtoto ambaye kama hakuangaliwa, anaweza kupelekea maafa dhidi ya jamii hii anayoonekana kuichukia.
Waswahili husema kimya kimoja kina thamani zaidi ya maropoko elfu moja. Alichokiropoka Doyo kinadhihirisha kwamba mbele ya chuki iliyojaa moyoni mwake dhidi ya jamii hii ya Kipemba, humfanya asahau kwamba miongoni mwa anaowachukia hukaa nao meza moja wakapanga mipango ya chama chao.
Yumkini, awali alikuwa akiwachukia kwa siri na asingependa wajuwe, lakini sasa Mungu amewaonesha kwamba ingawa anaowachekea hadi gego la mwisho, moyoni mwake ana sumu mbaya dhidi yao. Licha ya kuwa la kuchukiwa Wapemba halitakuwa ajabu iliyoanzwa naye, lakini isingependelewa kuendelezwa na kijana wa kisasa mfano wake, hasa kama kweli yuko kwenye siasa za mageuzi na kama jina la chama chake linavyosema kuwa ni cha umoja kwa ajili ya mageuzi ya kidemokrasia. Mageuzi ya kidemokrasia penye chuki hayawezi kuwepo, wala umoja penye kauli za kipuuzi kama hii hauwezi kujengwa.
Neno langu la mwisho kwake, ni kuwa sisi Wapemba tumemsikia na maandishi yake twayaweka kwenye kumbukumbu zetu. Ipo siku tutamfunulia ayasome. Siku ya baya lijalo likatutokezea, tutakuwa na ushahidi wa maandishi mahakamani, iwe ya kidunia au ile ya haki isiyokosea, mbele ya Allah!
TANBIHI: Mwandishi wa makala hii ni mwandishi wa habari wa kujitegemea.
Filed under: Siasa
