Mzee Aboud Jumbe Mwinyi, aliyewahi kuwa rais wa Zanzibar, makamu rais wa Tanzania, makamu mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na – kubwa kuliko yote – kiongozi aliyefunguwa milango ya demokrasia baada ya Mapinduzi ya 1964 na hatimaye kuja kupigania muundo sahihi wa Muungano – ametangulia mbele ya haki akiwa na umri usiopunguwa miaka 95. Umri huu ni wachache miongoni mwetu kuweza kuufikia. Allah ampokee mzee huyu na kulifanya kaburi lake liwe ni miongoni mwa mabustani ya peponi yanayopitiwa na ile mito ya maziwa na asali kama ilivyoahidiwa kwa waja wema.
Jicho langu linamtazama Mzee Jumbe kama samaki aliyekufa majini huku akiwa amejaa mengi ya kusema mdomoni lakini hakuyasema. Jicho langu linamtazama kama mfungwa aliyefungiwa gerezani na kutowahi kuionja nje tangu alipoingizwa mwaka 1984 hadi anafikwa na umauti. Jicho hili linamtazama kama shujaa aliyekubali kufa na msimamo ambao aliubeba kwenye dhamiri yake bila kuusaliti hadi pale kifo kilipomtenganisha baina ya sisi na yeye. Hali hii inaashiria kwamba ingawa Mzee Jumbe amefariki dunia, lakini aliyoyaamini yataendelea kuwa hai daima dawamu hadi haki aliyoipigania kwa ajili ya Zanzibar ipatikane, madhali tu wapo Wazanzibari wanaoamini juu ya haki hiyo.
Na Ahmad Abu Faris
Nilianza kumjuwa Mzee Jumbe wakati nikiwa mdogo sana miaka ile ya ’70 na mwanzoni mwa ’80. Kwanza ilikuwa kupitia magazeti na picha za kalenda mbalimbali zilomuonesha akishiriki shughuli za kimaendeleo visiwani Zanzibar. Hatimaye, mwanzoni mwa miaka ya ’80, Mzee Jumbe alitembelea kijijini kwetu kukagua shughuli za kilimo kwenye bonde maarufu kisiwani Pemba, bonde la Makwararani. Pamoja na udogo niliokuwa nao kipindi hicho, bado nakumbuka tukio la Mzee Jumbe kumtunza pesa mpiga msewe mashuhuri katika wilaya ya Micheweni, Mzee Bin Malengo, ambaye alikuwa gwiji wa ngoma hii. Tendo hili lilikuwa la heshima kubwa kwa gwiji huyo kiasi cha kuwa gumzo kwenye wilaya nzima ya Micheweni, na likawa kichocheo cha ngoma hii kuenziwa na kuendelezwa hadi leo hii, tofauti na ngoma nyingine nyingi za kiutamaduni zilizokufa.
Mara nyingi misimamo ya kutetea umma ina madhara yake na historia inaonesha kwamba imewaponza wengi, Mzee Jumbe akiwa miongoni mwao. Mengi tumesimuliwa kuhusu Mzee Jumbe lakini kubwa likiwa lile la kutofautiana kimsimamo na mtawala wa mwanzo wa Tanganyika huru, suala ambalo lilipelekea Mzee Jumbe kuvuliwa nyadhifa zake za uongozi na hatimaye kuwekwa kwenye kizuwizi cha ndani kwenye kijiji chake alichokiita Mji Mwema kule Kigamboni.
Tofauti na ilivyo sasa, eneo hili lilikuwa pori lisilo na huduma za msingi kwa binadamu kutokana na jiografia yake wakati huo. Mji Mwema ya enzi ya Mwalimu Julius Nyerere si Mji Mwema ya leo. Wakati Mzee Jumbe akiwekwa kwenye kizuwizi cha ndani na waliomzidi nguvu, eneo hili lilikuwa pori lilojaa kenge, chatu na majoka. Lilikuwa eneo gumu kufikika kutokana na kutegemea zaidi pantoni ambazo hazikuwepo kama ilivyo sasa. Hivyo ingawa haisemwi waziwazi, bado hali halisi inathibitisha kile kifichwacho ambacho mzee wetu alisukumiwa na kisha kutelekezwa huko kwenye pori la Mji Mwema.
Jambo moja limenipa faraja na kunifanya nipate nguvu na uthubutu wakumuita Mzee Jumbe kwa jina la shujaa. Jumbe ni shujaa aliyesimama bila kutetereka kwenye msimamo wake pahusupo maslahi ya Zanzibar. Ameuthibitishia ulimwengu kwamba ingawa aliondolewa kwa nguvu madarakani , bado uamuzi huo wa kibabe haukumfanya afifie na kupoteza mapenzi yake kwa Zanzibar na Wazanzibari. Ndipo akiwa na akili timamu, alipothubutu kuwaita viongozi kadhaa wakiwemo wanasheria wa serikali na kuandika wasia wake kwa umma wa wapi azikwe, vipi azikwe na kama mtu aliyefikia kuwa raisi wa nchi huru ya Zanzibar, kipi afanyiwe.
Wengi hawafahamu maana na mantiki ya uamuzi huu wa Mzee Jumbe. Lakini ukweli ni kwamba Mzee Jumbe amefariki akiwa na kinyongo kibaya nafsini mwake kutokana na dhulma aliyofanyiwa na watawala wenzake kwa sababu tu ya mapenzi yake makubwa kwa nchi yake Zanzibar. Ameandika waraka huu kwa lengo la kujiweka mbali na wanafiki ambao walimfisidi jana, akijuwa kwamba ipo siku wangejileta mbele yake kuonesha kwamba wako naye hali ya kuwa walijitenga naye mbali enzi za mateso yake wakati akiwa hai. Alijuwa kwamba ipo siku wangejitokeza na mizinga yao wakiamini ndio heshima kwake, ilihali jana tu walikuwa chui waliotamani roho yake mbichi. Hili Mzee Jumbe alilijuwa na akaweka utaratibu wa kuwakataa mapema tangu yungali na akili zake timamu. Hongera Mzee Jumbe. Ujumbe wako umefika na wameusoma.
Kubwa zaidi ni kuwa Mzee Jumbe ameidhihirishia dunia kwamba Mji Mwema hapakuwa mahali alipopachaguwa kwa ridhaa ya nafsi yake bali alitwezwa nguvu kuwa hapo. Hapa aliishi muda mrefu wa maisha yake, lakini hakuishi kwa ridhaa yake bali alilazimishwa – sichelei kusema – kwa vitisho na vitimbi vya kumfanya ajae unyonge wa kupitiliza moyoni mwake. Ndio sababu, ndani ya waraka ule aliweka bayana kwamba ardhi aipendayo toka kwenye chembe ya moyo wake, ni ardhi tukufu ya Zanzibar.
Alhamdulillah, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi amefia uhamishoni Mji Mwema na amezikwa kwenye ardhi tukufu aliyoipenda ya Migombani katika mji mtakatifu wa Zanzibar. Je, hii ni aibu au si aibu kwa waliomchukuwa na kwenda kumsokomeza maporini kule Mji Mwema enzi hizo, kwa sabababu tu ya kupigania maslahi ya Zanzibar na Wazanzibari?
Wakati wa maziko ya mzee wetu kuna tukio jingine kubwa ambalo lilijiri. Hili ni tukio la Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) na makamu wa kwanza mstaafu wa rais wa Zanzibar, kuukataa mkono wa Dk. Ali Mohamed Shein.
Hili si tukio la kawaida kwa hadhi na heshima za watu hawa kitaifa na kimataifa, bali ni ishara mbaya ambayo haipaswi kuachwa iendelee kuwepo. Ni tukio litowalo ishara kwamba huko tuendako ni kubaya zaidi kama tutashindwa kujitowa hadharani na kuileta pamoja Zanzibar. Ni tukio litowalo ishara kwamba Wazanzibari wameparaganyika na lolote laweza tokea ikiwa hali ya sasa ya Zanzibar haikutafutiwa suluhisho lake. Lakini mbaya zaidi, hili ni tukio lenye ujumbe wa aina yake kwa Dk. Shein na serikali yake kwamba kama wanadhani wanaogopwa,wanajidanganya.
Binafsi siitazami hali hii kwa jicho la kawaida, bali nimeingia ndani kulitafiti na hapa naeleza wazi kwamba vifo vitaendelea kutukutanisha kama ilivyosadifu jana, lakini huko mbele twendako, wenye mizinga na vifaru na miguvu yao hiyo watashuhudia wenye nguvu ya umma wakijitenga mbali nao na hivyo kifo kimoja kitakuwa na matanga mawili – la wenye vifaru na mizinga kwao na wale wenye nguvu ya umma ambao ndio wengi kwao! Hilo halipo mbali na punde tutalishuhudia kwani tumedharau kutenda haki kwa wanaostahili haki.